Uzinduzi Wa Kamati Ya Ushauri Wa Kisekta IAA

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) Dkt. Mwamini Tulli amezindua rasmi Kamati ya Ushauri wa Kisekta (Industrial Advisory Committee), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mapinduzi ya Kiuchumi (HEET).

Akizindua kamati hiyo Dkt. Mwamini Tulli ameipongeza serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan Pamoja na Benki ya Dunia (WB) kwa kuanzisha mradi wa HEET ambao umezinufaisha taasisi mbalimbali za kielimu IAA ikiwa moja wapo.

Dkt. Tulli amesema moja kati ya majukumu ya kamati hiyo ni kutoa ushauri kwa Chuo kuhusu mitaala, kuwezesha wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo, kutoa mapendekezo ya wabobezi watakaowapa uwezo wanafunzi kitaalamu, pamoja na kuwa mabalozi wa IAA na daraja la mawasiliano kwa jamii.

Pia Dkt. Tulli amethibitisha kuwa wao kama Baraza la Uongozi IAA watahakikisha wanatoa ushirikiano wa dhati kwa wajumbe wa kamati hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao, ili kufikia malengo kama Chuo na kutimiza matakwa ya mradi na wizara kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha IAA Prof. Eliamani Sedoyeka ameishukuru serikali kwa kuwapa fedha takribani Bil. 47 kupitia mradi wa HEET ambazo zitawasaidia kutoa elimu bora na kuandaa vijana wenye weledi watakaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Prof. Sedoyeka ameongeza kuwa fedha walizozipata kupitia mradi huu wamezielekeza zaidi katika kuboresha miundombinu ya Chuo, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji, kushughulikia masuala ya jinsia na elimu jumuishi pamoja na mengine mengi ambayo yatawawezesha kuendelea kutoa elimu bora.

“Kama Chuo tutaendelea kutoa Elimu inayojibu mahitaji ya jamii, tutaendelea kufanya tafiti ambazo matokeo yake yatatumika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii pia” alisema Prof. Sedoyeka

Nae mwakilishi kutoka UN WOMEN Bi. Lilian Liwa ambae pia ni mjumbe wa kamati hiyo amesema watashirikiana na IAA ili kuhakikisha mradi unawasaidia vijana kupata elimu bora ili kuinufaisha jamii ya watanzania.